Wananchi waeleza changamoto ujenzi wa barabara za TACTIC
7 January 2025, 10:56 am
Wananchi waeleza changamoto zitokanazo na matengezo na ujenzi wa barabara zenye urefu wa KM 17 kupitia mradi wa TACTIC unaofadhiliwa na benki ya dunia.
Na: Edga Rwenduru – Geita
Wananchi wanaoishi maeneo unapofanyika ujenzi wa mradi wa barabara zenye urefu wa kilometa 17 kupitia TACTIC manispaa ya Geita wameiomba serikali kumuelekeza mkandarasi anayetekeleza mradi huo kufukia mashimo yaliyochimbwa wakati wa ujenzi wa kwani yanapelekea changamoto kwa wakazi hao.
Wakizungumza na storm FM Januari 05, 2024 wamesema toka ujenzi wa barabara hizo uanze nyumba tisa tayari zimebomoka kutokana na maji ya mvua kuelekezwa kwenye makazi yao huku baadhi ya wanafunzi wa shule za msingi wakishindwa kuvuka baadhi ya maeneo kutokana na barabara kuwa na mashimo yaliyojaa maji.
Diwani wa kata ya Nyankumbu John Lunyaba Mapesa amesema licha ya serikali kutoa fedha kwaajili ya ujenzi wa barabara hizo zenye urefu wa kilometa 17 changamoto ya kutokamilika kwa mradi huo inatokana na uzembe wa mkandarasi.
Mkuu wa wilaya ya Geita Hashim Komba amesema serikali hairidhishwi na uwezo wa mkandarasi na kuwaahidi wananchi kuchukua hatua za haraka ili kutatua changamoto hiyo.