Wachezaji zaidi ya 20 waikimbia Biashara United
27 December 2024, 9:50 pm
Wakati ligi ya Championship ikielekea katika mzunguko wa pili timu ya Biashara United inakabiliwa na changamoto ya kiuchumi.
Na Mrisho Sadick:
Wachezaji zaidi ya 20 na benchi la ufundi la timu ya Biashara United ya mkoani Mara wameikimbia timu hiyo kutokana na ukata wa fedha ya uendeshaji.
Mkurugenzi wa ufundi wa timu hiyo Madenge Omary amebainisha hayo leo disemba 27,2024 Mkoani Geita baada ya timu hiyo kufungwa bao 5-0 na Geita Gold FC katika mwendelezo wa ligi ya Championship na timu hiyo iliingia uwanjani ikiwa haina mchezaji hata mmoja wa akiba.
Amesema Kutokana na Changamoto hiyo wamelazimika kutumia wachezaji wa timu ya vijana kwa ajili ya kuinusuru hata hivyo amesema matatizo hayo yapo mbioni kumalizika kwakuwa wapo kwenye mazungumzo na mdhamini mpya.
Baada ya Geita Gold FC kuibuka na ushindi wa bao 5 – 0 , kocha mkuu wa Geita Gold FC Aman Josia amesema baada ya kupoteza ugenini dhidi ya Mbeya City nakutoa sare dhidi ya Songea United walijiandaa kikamilifu kuwavaa biashara na wamefanikiwa kupata ushindi mnono.
Kwa matokeo hayo Geita Gold FC imefikisha alama 30 ikiwa imecheza michezo 14 na ipo nafasi ya 2 kwenye msimamo wa championship Nyuma ya Mtibwa Sugar.