Tazama lori lilivyopata ajali eneo la round about Geita
19 December 2024, 9:49 am
Mkuu wa kitengo cha usalama barabarani mkoa wa Geita ametoa rai kwa watumiaji wa vyombo vya moto kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kupunguza ajali zinazotokana na ukiukwaji wa sheria hizo.
Na: Evance Mlyakado – Geita
Gari kubwa la mizigo aina ya lori limepata ajali ya kutumbukia kwenye mtaro na kuziba barabara katika eneo la round about mjini Geita hali iliyopelekea barabara kufungwa kwa muda wa saa 4 ili kuweza kuliondoa.
Ajali hiyo imetokea Disemba 18, 2024 ambapo Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoani Geita Mrakibu wa jeshi la polisi Aloyce Jacob amesema ajali hiyo imetokea kipindi ambapo dereva wa lori alikuwa akijaribu kuikwepa pikipiki ambayo ilitokea ghafla na kupelekea gari hilo kupoteza mwelekeo.
Afande Aloyce Jacob amesema ajali hiyo haijasababisha madhara yoyote kwa binadamu huku akiwataka madereva kuwa makini kuzingatia alama za barabarani kwa umakini mkubwa.
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo wamesema ajali hiyo imesababisha foleni kubwa ya magari kwani iliziba barabara na kupelekea baadhi ya magari kulazimika kupita barabara za mitaa.
Aidha Afande Jacob ametoa rai kwa madereva wote wa vyombo vya moto kuwa makini sana wawapo barabarani hususani kipindi hiki cha mwisho wa mwaka na kuhakikisha wanazingatia sheria za usalama barabara ili kuepusha ajali zisizo za lazima.
Gari hilo lilivutwa na kutolewa barabarani na mtambo maalumu kutoka mgodi wa Geita Gold minning limited (GGML).