GGML kuendelea kuwajibika kwa jamii Geita
5 December 2024, 12:40 pm
GGML yasema bado iko bega kwa bega na wananchi kwa kushiriki katika shughuli mbalimba za maendeleo katika jamii bila kuchoka.
Na Mrisho Sadick:
Mgodi wa Geita Gold Mining Limited (GGML) umewahakikishia wananchi wa mkoa wa Geta kuwa utaendelea kuwajibika ipasavyo katika shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo elimu , afya ,miundombinu ya barabara pamoja na uwezeshaji wananchi kiuchumi kupitia uwajibikaji wa makampuni kwa jamii (CSR).
Kauli hiyo imetolewa na mkurugenzi mtendaji wa mgodi huo Duran Archery Disemba 04,2024 katika hafla ya kufunga mwaka 2024 iliyowakutanisha wenyeviti wa serikali za mitaa wapya na wastaafu, madiwani, watendaji wa kata na viongozi wa dini iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Saint Aloysius Kata ya Kalangalala mjini Geita, mgodi wa GGML umeelezea dhamira yake ya kuendelea kushirikiana na jamii huku ikiwapongeza wananchi na viongozi kwa kuwapa ushirikiano kuanzia mwezi januari hadi disemba mwaka huu.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita, Nicholous Kasendamila akiwa katika hafla hiyo amewataka wananchi kuendelea kuunga mkono mgodi huo huku akiiomba GGML kukamilisha miradi ya CSR iliyobaki ili kuleta manufaa endelevu kwa jamii ya Geita.
Mwakilishi wa Mbunge wa Jimbo la Geita mjini amepongeza juhudi za mgodi huo kutoa ajira za ulinzi kwa vijana wanaozunguka eneo hilo huku akiomba uendelee kuboresha maslahi ya vijana hao ili waweze kunufaika wao , familia zao na serikali za mitaa yao.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo Mkuu wa Wilaya ya Geita, Hashim Komba, amesisitiza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na mgodi wa GGML kwakuwa umekuwa chachu ya maendeleo katika mkoa wa Geita na taifa kwa ujumla, kwa kuleta mafanikio katika sekta za uchumi, ajira, na huduma za kijamii.
Hafla hii ilikuwa ni ishara ya juhudi zinazofanywa na GGML katika kuhakikisha maendeleo endelevu na ushirikiano mzuri na jamii, huku ikiendelea kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya mkoa na taifa kwa ujumla.