Akutwa amefariki mlangoni kwa jirani yake Msalala road
28 November 2024, 10:15 am
Mwili wa mwanaume aliyetambulika kwa jina moja la Tumaini umekutwa mlangoni kwa jirani yake huku chanzo cha kifo chake kikiwa bado hakijafahamika.
Na: Amon Mwakalobo – Geita
Mwanaume mmoja anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 35 aliyejulikana kwa jina moja tu la Tumaini maarufu kama Kitale amekutwa amefariki mlangoni kwa jirani yake asubuhi ya tarehe 27/11/2024 huku chanzo cha kifo chake kikiwa hakijafahamika.
Tukio hilo limetokea katika mtaa wa Msalala road halmashauri ya mji wa Geita katika ubalozi wa Kuruthum Ahmada ambapo kwa mujibu wa Balozi huyo anasema mwanaume huyo alikuwa hana mahali pa kuishi ambapo aliletwa na wazazi wake kutoka Kigoma kwaajili ya masomo ambapo aliacha shule na kuingia mitaani.
Jirani yake na Kitale amesema aliamka asubuhi na kukuta Kitale amelala mlangoni kwake na ndipo akaamua kuanza kuamsha watu pamoja na Balozi.
Aliyekuwa mwenyekiti wa serikali ya mtaa huo ambaye pia jana amechaguliwa kuwa mwenyekiti kwa mara nyingine Sostenes Kalist ameeleza alitoa taarifa Jeshi la polisi kwaajili ya hatua zaidi.