Kanisa Katoliki, GGML wawaibua watoto wenye ulemavu Geita
18 November 2024, 6:16 pm
Katika jamii hususani mikoa ya kanda ya ziwa bado kuna changamoto ya watoto wenye ulemavu kuendelea kufichwa huku imani potofu ikitajwa kuwa sababu.
Na Mrisho Sadick:
Kanisa Katoliki Jimbo la Geita kwa kushirikiana na mgodi wa GGML limefanikiwa kuwaibua watoto wenye ulemavu zaidi ya 5,000 waliyokuwa wamefichwa majumbani katika halmashauri sita za mkoa wa Geita kwa lengo la kuwasaidia kupata haki za msingi ikiwemo elimu.
Askof wa kanisa katoliki jimbo la Geita Flavian Kasala amesema hayo leo Novemba 18,2024 wakati akikabidhi vifaa saidizi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika kituo cha shule ya msingi Mbugani nakwamba kanisa hilo kwa kushirikiana na mgodi wa GGML na wadau wengine linatekeleza mradi wa miaka mitatu wa kuondoa imani potofu kuhusu watoto wenye ulemavu kwakuwa idadi kubwa ya watoto hao ukanda wa ziwa wanafichwa majumbani.
Mratibu wa mradi huo Joseph Masawe amesema mradi huo unatekelezwa katika kata 12 kwenye halmashauri sita za mkoa wa Geita ili kupata takwimu halisi za watoto wenye ulemavu wa kuanzia mwaka 0-12 ili kutambua namna ya kuwasaidia kulingana na ulemavu wao huku diwani wa kata ya Kalangalala Prudence Temba akilipongeza kanisa hilo kwa hatua hiyo.
Kwa upande wake mwakilishi wa mkurugenzi wa Mgodi wa GGML Elibariki Jambau amesema mgodi huo kwa kushirikiana na World Gold Council wamejikita katika kushughulikia changamoto kubwa katika jamii zinazo wakabili watoto wenye ulemavu katika mkoa wa Geita na kwingine.
Awali akitoa taarifa ya maendeleo ya kituo cha wanafunzi wenye mahitaji maalmu mwalimu mkuu wa shule ya msingi Mbungani amesema kituo hicho kina wanafunzi 160 nakwamba wengi wao wanaendelea kupata ujuzi mbalimbali huku afisa elimu msingi wa halmashauri ya mji wa Geita Sostenes Mbwilo akilipongeza kanisa katoliki kwa msaada huo.