REA kusambaza umeme vitongoji 105 Geita
23 October 2024, 3:57 pm
Umeme vijijini umekuwa chachu na mabadiliko ya haraka kwa uchumi wa wananchi huku serikali ikiahidi kufikisha huduma hiyo kila kitongoji.
Na Mrisho Sadick:
Wakala wa nishati vijijini (REA) umeanza Kusambaza Umeme kwenye vitongoji 105 vya majimbo saba (7) ya mkoa wa Geita ikiwa ni mkakati wa serikali wa kuhakikisha kila kijiji na vitongoji vyake vinafikiwa na umeme.
Msimamizi wa miradi ya REA mkoa wa Geita Mhandisi Dominick Mnaa akimtambulisha mkandarasi anaetekeleza mradi huo kwa mkuu wa mkoa wa Geita kutoka kampuni ya CCC Industrial Commercial Limited ya nchini China Oktoba 22,2024 Ofisini kwake Magogo mjini Geita amesema Mradi huo utakuwa wa miaka miwili kuanzia sasa.
Mwakilishi wa kampuni ya CCC (Beijing) Industrial and Commercial Ltd hapa nchini Tanzania Bi. Carol Wang amesema kampuni hiyo imejipanga ili kukamilisha Mradi huo kwa wakati.
Mkuu wa mkoa wa Geita Martine Shigela amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kudhamiria kufikisha umeme kwenye vitongoji vyote huku akiwataka viongozi wa serikali za mitaa unakopita mradi huo kumpa ushirikiano mkandarasi.
Mkoa wa Geita una kata 122, vijiji 486 na vitongoji 2,195, ambapo hadi sasa jumla ya kata 121, vijiji 483 na vitongoji 1,017 vimeshafikiwa na huduma ya umeme.