Rais Samia atoa milioni 50 kwa wanawake Geita
22 October 2024, 9:59 pm
Serikali imeendelea kuweka nguvu kwa wanawake wanaofanya shughuli katika migodi ya uchimbaji wa madini ya dhahabu ili kuwainua kiuchumi.
Na Mrisho Sadick:
Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassani ametoa kiasi cha shilingi milioni 50 kwa taasisi ya Wanawake na Samia mkoa wa Geita kwa lengo la kuwaongezea mtaji wa kuendeleza biashara yao ya kupika chakula kwa wafanyakazi wa Shirika la Madini la Taifa STAMICO katika mgodi wa GGML.
Akikabidhi risiti za kiasi cha fedha kilichowekwa katika akaunti ya taasisi hiyo na Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt Samia Sukuhu Hassan Oktoba 21,2024 Mkuu wa mkoa wa Geita Martine Shigela amewataka kutumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa ili kukuza mtaji na kupanua wigo wa kutoa huduma ya chakula kwa makampuni mengine.
Mwenyekiti wa Taasisi hiyo Adelina Kabakama amesema wanatoa huduma ya chakula kwa watumishi zaidi ya 100 wa shirika la madini la taifa STAMICO ambapo wamemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwasaidia kutatua changamoto ya mtaji.
Hivi karibuni akiwa mkoani Geita kwenye hafla ya kufunga maonesho ya saba ya teknolojia na uwekezaji katika sekta ya madini Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan aliahidi kuendelea kuwashika mkono wanawake wanaofanya kazi migodini.