Waziri Mavunde atembelea kijiji cha Ushirika, atoa maagizo kwa TAKUKURU
9 October 2024, 10:29 am
Waziri wa Madini Antony Mavunde ameendelea na ziara za ndani ya mkoa wa Geita akitembelea maeneo mbalimbali sambamba na kuzungumza na wachimbaji wadogowadogo.
Na: Edga Rwenduru – Geita
Waziri wa madini Anthony Mavunde ameiagiza Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa nchini TAKUKURU wilaya ya Mbogwe kuharakisha uchunguzi wa viongozi wanaotuhumiwa kuhujumu fedha za ujenzi wa kituo cha afya Ushirika kilichopo wilayani Mbogwe mkoani Geita jambo ambalo limesababisha ujenzi wa kituo hicho kusimama.
Ametoa maagizo hayo Oktoba 08, 2024 mara baada ya kuweka jiwe la msingi katika mradi huo ambapo amesema mpaka sasa ujenzi wa kituo hicho cha afya umegharimu zaidi ya shilingi milioni 534 na inahitajika zaidi ya milioni 63 ili kukamilisha ujenzi wa mradi huo.
Mkuu wa mkoa wa Geita Mhe. Martine Shigela ameeleza hatua zilizopigwa katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za kiafya huku Mbunge wa Jimbo la Mbogwe Nicodemas Mganga akieleza mchakato ulivyokuwa katika ujenzi wa kituo hicho.
Akisoma taarifa ya mradi huo Afisa mtendaji wa kata ya Ushirika Bw. Juma Luchagula amesema kituo hicho kitakapo kamilika kitaweza kuhudumia zaidi ya wananchi elfu 35.
Baadhi ya wakazi wa kata ya Ushirika Agathe Richard na Magreth Masanja wanabainisha changamoto wanazozipata kutokana na kutokamilika kwa wakati ujenzi wa kituo hicho.