Wakazi Buhalahala wapongeza uwekwaji taa za barabarani
28 September 2024, 10:27 am
Mkoa wa Geita umeendelea kukua na kuimarika kupitia nyanja mbalimbali, hivyo uboreshaji wa miundombinu ni muhimu katika ukuaji wa uchumi.
Na: Kale Chongela – Geita
Wakazi wa kata ya Buhalahala halmashuri ya mji wa Geita wameipongeza serikali kwa kuendelea kuboresha miundombinu kwa kuweka taa pembezoni mwa barabara kuu.
Wakizungumza Septemba 27, 2024 baadhi ya wakazi wa mtaa wa Mwatulole uliopo katika kata hiyo wamesema kuwepo kwa taa hizo zitawasaidia wananchi wa eneo hilo hasa watembea kwa miguu.
Aidha wananchi wameendelea kueleza kuwa taa hizo ni chachu kubwa katika hatua ya ukuaji wa kiuchumi kwa mkoa na taifa kwa ujumla.
Akizungumza kwa njia ya simu mtaalumu kutoka wakala wa Barabara mkoani Geita (TANROADS) Mhandisi Fedrick Mande amesema ili taa hizo ziweze kudumu kwa muda ipo haja kwa kila mwananchi kutoa ushirikiano katika kulinda miundombinu ya barabara ili kuepukana na hasara zisizokuwa za lazima.