Storm FM

Dereva anusurika kifo baada ya kujeruhiwa na wasiojulikuana Geita

16 August 2024, 1:49 pm

Issa Lameck, dereva bodaboda aliyejeruhiwa eneo la kichwani baada ya kuvamiwa na watu akiwa na abiria wake katika pori la Bugurula. Picha na Edga Rwenduru

Matukio ya madereva pikipiki maarufu bodaboda kuvamiwa na kujeruhiwa huku baadhi yao wakiporwa pikipiki yanaacha hofu kwa madereva huku wakiomba mamlaka za serikali kuwasaidia.

Na: Amon Mwakalobo – Geita

Kijana ambaye amefahamika kwa jina la Issa Lameck mkazi wa kata ya Nyankumbu ambaye anafanya kazi ya boda boda katika kijiwe cha Nendeni na Amani mjini Geita amenusurika kifo baada ya kujeruhiwa na watu wasiojulikana katika barabara inayopita katika pori la Bugurula.

Akizungumza na Storm Fm Issa amesema tukio hilo limemtokea Agosti 13, 2024 majira ya saa 12 alfajiri alivyotoka asubuhi akiwa na mteja wake kama anavyoelezea.

Sauti ya Issa Lameck

Baadhi ya madereva wanaofanya naye kazi wamesema kwa sasa hawana amani kabisa kwani hata wanapoondoka majumbani kuelekea eneo hilo lazima waage familia zao kuwa wanaweza kurudi ama wasirudi na kuiomba serikali ya mkoa wa Geita kuwasaka waharifu hao.

Mwenyekiti wa bodaboda kata ya Kalangalala halmashauri ya mji wa Geita amesema matukio hayo yamekuwa yakiripotiwa polisi lakini hawaoni utekelezaji wa hatua zozote hivyo kuiomba serikali iwatatulia kero hiyo.

Sauti ya mwenyekiti
Mkuu wa mkoa wa Geita Martine Shigela katika mkutano wa katibu mkuu wa CCM bara Dkt. Emmanuel Nchimbi (hayupo pichani)

Mkuu wa mkoa wa Geita Martine Shigela ambaye alikuwa katika mkutano wa katibu mkuu wa CCM bara Dkt. Emmanuel Nchimbi uliofanyika eneo la Nyankumbu Agosti 13, 2024 alimuahidi katibu mkuu kuwa atashughulikia kero hiyo kwa haraka zaidi.

Sauti ya RC Geita