Wakazi Nyarugusu walalamika ujenzi wa barabara kusimama
1 August 2024, 2:17 am
Wakazi wa kata ya Nyarugusu Wilaya ya Geita wamelalamikia hali ya kusimama kwa ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita moja.
Na: Kale Chongela – Geita
Malalamiko ya wanachi hao yamekuja kufuatia usumbufu ambao wananchi hao wanaeleza kuupata hususani watumiaji wa vyombo vya moto.
Wameeleza hayo Julai 30, 2024 wakati wakizungumza na Storm Fm ambapo wameeleza kuwa ni zaidi ya siku 60 ujenzi huo umesimama jambo ambalo linawapa wakati mgumu.
Baadhi ya madereva wa boda boda katika eneo hilo wanaeleza kuwa baada ya ujenzi huo kusimama barabara imefugwa huku akiiomba serikali kufungua barabara hiyo ili iweze kuwarahisishia kazi yao.
Oscar Fredrico ni katibu wa egesho la bodaboda la Nyarugusu anaiomba serikali kuweza kufungua barabara hio ili kuwasaidia watumiaji kuondokana na changamoto ya sasa.
Kutoka wakala wa barabara TANROADS mkoa wa Geita mhandisi Fredrick Mande akizungumza kwa njia ya simu amesema barabara hiyo ina urefu wa kilomota 1 na miongoni mwa sababu zilizopelekea kusimama kwa ujenzi huo ni fedha kuchelewa hali iliyopelekea mkandarasi kusimama kwa muda hadi fedha itakapopatikana ndipo ujenzi utaendelea.