Storm FM

DC Kingalame akaa mguu sawa miradi ya mwenge

15 July 2024, 12:54 pm

Mkuu wa wilaya Nyang’hwale Grace Kingalame akiwa na watendaji wa Halmashauri hiyo katika ukaguzi wa miradi ya mwenge wa uhuru. Picha na Mrisho Sadick.

Wilaya ya Nyang’hwale imeendelea kujiimarisha katika sekta mbalimbali ikiwemo za afya , maji , elimu, miundombinu ya barabara, nakutumia fursa ya nishati ya umeme kukuza uchumi wa wananchi wake.

Na Mrisho Sadick:

Serikali kupitia Wizara ya nishati imefanikiwa kufikisha umeme kwenye vijiji vyote na migodi ya wachimbaji wadogo wa madini  ya dhabau katika  wilaya ya Nyag’hhwale Mkoani  Geita.

Kauli hiyo imetolewa na mkuu wa wilaya ya Nyanghwale Grace Kingalame Julai 13,2024 katika ziara yake ya uhakiki wa miradi itakayofikiwa na mwenge wa uhuru pamoja na kuangazia shughuli za wachimbaji wadogo waliofikiwa na nishati hiyo wilayani humo ambapo amesema serikali imefikisha umeme kwenye vijiji vyote 62 na vitongoji 88 kati ya 273 vya wilaya hiyo.

Sauti ya DC Kingalame
Mradi wa umeme kwa wachimbaji wadogo wa kijiji cha Nyamalapa wilayani Nyang’hwale. Picha na Mrisho Sadick

Kaimu mejena wa TANESCO wilaya ya Nyanghwale Richard Maduhu amesema mradi wa kufikisha umeme kwa wachimbaji wadogo katika kijiji cha Nyamalapa  umegharimu milioni 78.9 wenye urefu wa kilometa 1.27 kutoka katika laini ya msongo wa kati wa umeme  na wachimbaji hao wameanza kuutumia.m

Sauti ya Kaimu Meneja TANESCO

DC Kingalame mbali nakutembelea miradi ya Afya , Maji , Vijana na barabara ametembelea shule ya sekondari ya kisasa iliyojengwa kwa gharama ya zaidi ya milioni 500  huku  mkuu wa shule hiyo Yona Mbiha akiipongeza serikali nakuomba kutatua changamoto ya barabara ya kufika shuleni hapo kwani wanalazimika kuzunguka umbali mrefu ili hali kuna njia ya mkato ambayo ina hitaji marekebisho.

Muonekano wa shule ya sekondari ya kisasa ya kanegere wilayani Nyang’hwale. Picha na Mrisho Sadick

Katika hatua nyingine Kingalame amesema wameanza ukaguzi wa miradi 8 yenye thamani ya zaidi ya bilioni 4.5 itakayo pitiwa na mwenge wa uhuru ili kubaini changamoto zilizopo nakuzifanyia kazi  mapema kwa mategemeo ya kufanya vizuri zaidi kuliko mwaka jana.

Sauti ya DC Kingalame
Sehemu ya wachimbaji wadogo wa kijiji cha Nyamalapa waliofikiwa na nishati ya umeme . Picha na Mrisho Sadick