Maadhimisho ya siku ya idadi ya watu kitaifa yafanyika Geita
11 July 2024, 6:36 pm
Ongezeko la idadi ya watu duniani bado linaendelea kuacha maswali ya namna idadi hiyo itakavyoendana na ukuaji wa uchumi wa wananchi.
Na Daniel Magwina
Naibu Waziri ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Stanslaus Nyongo amewataka watendaji wa serikali nchini kutumia takwimu za idadi ya watu kupanga maendeleo endelevu kwa kuwa baadhi ya maeneo ukuaji wa idadi ya watu haiendani na ukuaji wa uchumi wa wananchi.
Mhe Nyongo ametoa maagizo hayo katika maadhimisho ya idadi ya watu duniani ambayo kitaifa yamefanyika mkoani Geita ambapo amesema mbali na mkoa huo kutajwa na Shirika la Idadi ya Watu kuwa na ongezeko kubwa la ukuaji wa idadi ya watu kwa mwaka, idadi hiyo imeanza kwenda na ukuaji wa uchumi.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela amesema uwepo ongezeko hilo la idadi ya watu mkoani humo imechechemua sekta mbalimbali katika maendeleo.
Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango anjela shayo amesema mkoa wa Geita unaongoza kwa takwimu za uzazi kwa asilimia 6.1 ikilinganishwa na kile cha kitaifa cha asilimia 8.1.
Msaidizi wa mwakilishi mkazi wa shirika la Kimataifa la Idadi ya watu duniani UNFPA Dkt Majaliwa Marwa amesema ili kuwe na ustawi wa maendeleo ya watu ni muhimu kutumia takwimu katika kuweka mipango endelevu.
Kila mwaka, tarehe 11 Julai, huadhimishwa Siku ya Idadi ya Watu Duniani iliyoanzishwa na Umoja wa Mataifa ili kuongeza uelewa wa umma kuhusu masuala yanayohusiana na matukio ya kidemografia.