Storm FM

RPC Geita akemea wanaume kupiga wake zao

30 May 2024, 11:15 am

Kamanda wa jeshi la polisi SACP Safia Jongo akizungumza na wananchi. Picha na Evance Mlyakado

Licha ya wadau, serikali na mashirika mbalimbali kukemea vitendo vya ukatili hususani kwa wanawake, bado baadhi ya wanaume katika kijiji cha Nyamtukuza wanaendeleza ukatili wa kupiga wake zao.

Na: Evance Mlyakado – Geita

Kufuatia kadhia hiyo, kamanda wa jeshi la polisi mkoani hapa, SACP Safia Jongo amekemea vikali wanaume wenye tabia za kupiga wake zao.

Akizungumza akiwa katika mkutano wa hadhara wa mkuu wa mkoa wa Geita, Martine Shigela katika kijiji cha Nyamtukuza wilaya ya Nyangh’wale mkoani Geita, kamanda Safia Jongo amekemea suala hilo na kusema lipo kinyume cha sheria.

Sauti ya RPC Geita

Baada ya agizo hilo kutolewa kwa wananchi waliojitokeza Katika mkutano huo, baadhi ya wanaume walionekana kutofurahishwa na kauli hiyo akiwemo Samson Manyakhenda hali iliyompelekea kuiwasilisha kero hiyo kwa mkuu wa mkoa wa Geita.

Sauti ya Samson Manyakhenda
Samson Manyakhenda akizungumza katika mkutano wa hadhara. Picha na Evance Mlyakado

Baada ya kuwasilishwa kwa kero hiyo, Mkuu wa mkoa wa Geita Martine Shigela akamuagiza Kamanda Jongo kurejea tena kufafanua kauli yake hiyo.

Sauti ya RPC Jongo

Baada ya ufafanuzi huo kutolewa, baadhi ya wanaume walianza kutawanyika katika mkutano huo ikiwa ni ishara ya kuonyesha kutoridhia juu ya suala hilo.