Mgogoro wa ardhi chanzo ujenzi wa kanisa kusimama Geita
29 May 2024, 1:59 pm
Migogoro ya ardhi hutajwa kupelekea changamoto mbalimbali ikiwemo kuvunjwa majengo, ujenzi kusimama na wakati mwingine watu hufikishana mahakamani ili kupata suluhu.
Na: Kale Chongela – Geita
Ujenzi uliokuwa ukiendelea wa kanisa la Pentekoste FPCT mtaa wa Mbugani kata ya Kalangalala mjini Geita umesimama kutokana na eneo hilo kuwa na mgogoro kati ya kanisa na shule.
Maamuzi hayo yamefanyika mara baada ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi wilaya ya Geita Bw. Robert Nyamaigolo kufika eneo hilo kufutia malalamiko ya muda mrefu ya wananchi wa eneo hilo juu ya eneo la shule kuporwa na kuanziswa ujenzi wa kanisa.
Askofu wa kanisa la FPCT mtaa wa Mbungani mchungaji Devid Nzumbi amesikitishwa na kitendo kilichofanyika cha ujenzi kusitishwa ili hali yeye anazo hati miliki za eneo hilo.
Afisa ardhi kutoka halmashauri ya mji wa Geita Bw. Mwizarubi Selestine amesimamisha ujenzi huo kufutia kuwepo kwa mgogoro hadi hapo mwafaka utakapopatikana.
Katibu wa malezi na mazingira jumuiya ya wazazi wilaya ya Geita Bw. Mapungo Paschal ametumia fursa hiyo kuwasihi afisa ardhi kujikita kutatua migogoro inayotokana na mipaka ya viwanja.