Mpanduji ajiua kwa kujichoma kisu kisa wivu wa mapenzi
25 April 2024, 10:30 am
Ingawa ni ngumu kuelewa sababu ya mtu kujaribu kujiua, watu wanaojaribu kujiua ndio wanajua ukweli wa jambo hilo, kwa mujibu wa Shirika la afya duniani (WHO),zaidi ya watu 700,000 hufariki kwa kujiua kila mwaka.
Na Ester Mabula – Geita
Mpanduji Mshingwa (46) mkazi wa kijiji cha Bwanga wilayani Chato mkoani Geita ambaye aliripotiwa miezi kadhaa iliyopita kunywa sumu na kunusurika, amejichoma kisu na kupoteza maisha akiwa nyumbani kwake.
Inaelezwa chanzo cha uamuzi huo ni ugomvi baina yake na Bwana Halawa (mganga wa jadi) ambaye pia ni mkazi wa kijiji hicho kwa madai ya kutembea na mke wake kwa kipindi cha mwaka mmoja wakifanikiwa kupata mtoto mmoja na ikielezwa kuwa kwa sasa ana ujauzito mwingine na kwamba mganga huyo wa jadi amekuwa akijigamba kuwa yeye ndio Nzagamba (dume la mbegu).
Katika jaribio la awali baada ya kunusurika kifo baada ya kunywa sumu Bw. Mpanduji (marehemu kwa sasa) akizungumza na Storm FM alieleza juu ya tukio hilo ambapo baada ya ugonvi wa mwanzo Halawa (mganga wa jadi) ametokomea kusikojulikana hadi hii leo.
Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Geita Kamishna Msaidizi mwandamizi wa polisi SACP Safia Jongo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuiasa jamii kuacha kujichukulia sheria mkononi pindi wapitiapo matatizo ya kifamilia na badala yake watumie njia sahihi kutatua changamoto hizo