Kufariki kwa mjamzito Busanda wananchi waiangukia serikali
16 April 2024, 3:49 pm
Uhaba wa vituo vya afya kwa baadhi ya maeneo ya mkoa wa Geita umeendelea kusababisha changamoto mbalimbali ikiwemo vifo vya akina mama wajawazito na watoto.
Na Edga Rwenduru – Geita
Wakazi wa kijiji cha Lubanda kata ya Busanda wilayani na mkoani Geita wameiomba serikali kuwasaidia zahanati iliyojengwa kwa nguvu za wananchi katika eneo hilo ianze kufanya kazi kwani tayari imekamilika na haitoi huduma.
Baadhi ya wakazi hao Marietha Thomas , Mayala Magili na Tatu Masele wamesema hayo wakati wakizungumza na Storm FM kufuatia tukio la mama mjamzito kufariki dunia baada ya kujifungulia njiani wakati anaelekea kituo cha afya Katoro kilicho umbali wa zaidi ya kilometa 10 kutoka katika kijiji hicho.
Mwenyekiti wa kijiji hicho Charles Lile amesema kinachokwamisha zahanati hiyo kutoa huduma mpaka sasa ni kutokamilika kwa jengo la watumishi ambalo linajengwa kwa kutumia fedha za CSR.
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Geita Karia Rajabu amesema ofisi yake haijapata taarifa ya uwepo wa tukio hilo nakuwataka viongozi wa kijiji hicho kuwasilisha maombi ya kuanza kazi kwa zahanati hiyo ili kuepukana na changamoto kama hiyo.
Mkuu wa wilaya ya Geita Hashim Komba hivi karibuni aliahidi kufanya kikao cha pamoja na wasimamizi wa miradi ya CSR ambayo imechelewa kukamilika kwa wakati licha ya fedha hizo kutolewa.