TADIO yazipiga msasa redio 10 za kijamii
15 April 2024, 5:11 pm
Redio za kijamii zimekuwa na manufaa makubwa hapa nchini kwa kuwa zinajikita kuangazia changamoto za wananchi moja kwa moja katika maeneo husika na kuzifikisha kwa mamlaka husika ili zipatiwe ufumbuzi.
Na Mrisho Sadick:
Jukwaa la Redio za Kijamii Tanzania TADIO limezikutanisha redio 10 za kijamii kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania kwa lengo la kuendelea kuzijengea uwezo wa namna ya kuandaa na kuweka maudhui ya habari yenye manufaa kwa jamii wanazozihudumia.
Mafunzo hayo ya siku mbili ambayo yameanza April 15 hadi 16 mwaka huu yanafanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kitange katika Hotel ya Royal Village Jijini Dodoma kwa kuzikutanisha redio za kijamii za Storm FM kutoka mkoani Geita , Dodoma FM kutoka Dodoma , Sengerema FM kutoka Mwanza , Mazingira FM kutoka Mara, Mpanda FM kutoka Katavi, Joy FM kutoka Kigoma, Uyui FM kutoka Tabora, Sibuka FM kutoka Simiyu, Karagwe FM kutoka Kagera na Jamii FM kutoka mkoani Mtwara.
Mhariri mkuu wa Redio TADIO Hilali Ruhundwa amesema mafunzo hayo yanalenga kuwaongezea uwezo wahariri, wasimamizi na waandishi wa habari kutoka kwenye vituo hivyo ili kuongeza weledi na ubunifu katika uendeshaji wa jukwaa hilo.
Akizungumza katika mafunzo hayo msimamizi wa vipindi wa Storm FM Ester Mabula amesema jukwaa hilo la Redio za kijamii limekuwa na manufaa makubwa kwakuwa linatoa wigo mpana kwa makundi yote kupata habari kwa njia ya sauti , picha na maandishi huku Adelnus Banenwa Mhariri wa Mazingira FM akisema jukwaa hilo limekuwa mkombozi kwao.
Kwa upande wake afisa miradi wa TADIO Saumu Ramadhani amesema jukwaa hilo lina wanachama zaidi ya 40 nakwamba mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo waandishi wa habari wa namna ya kuongeza kipato kupitia mtandao huo huku mkufunzi wa mafunzo hayo Amua Rushita amesema kupitia jukwaa hilo sasa redio za kijamii zimekuwa na ushindani mkubwa tofauti na hapo awali.