Kampuni ya Blue Coast yakarabati madarasa saba
10 January 2024, 7:16 pm
Wawekezaji wazawa waliyopo wilayani Geita wametakiwa kushirikiana na serikali kuondoa changamoto mbalimbali zilizopo kwenye sekta ya elimu kwenye maeneo waliyowekeza.
Na Mrisho Sadick – Geita
Wakazi wa Mtaa wa Nyamalembo Kata ya Mtakuja Halmashauri ya Mji wa Geita wameishukuru kampuni ya Blue Coast Investment kwa kukarabati vyumba saba vya madarasa na Ofisi mbili za walimu katika Shule ya Msingi Nyamalembo.
Wananchi hao wametoa pongezi hizo katika hafla ya kukabidhi madarasa hayo Shuleni hapo huku wakiwaomba wawekezaji wengine katika eneo hilo kusaidia ukarabati wa majengo chakavu yaliyobaki kwenye shule hiyo.
Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nyamalembo amesema kukamilika kwa ukarabati huo utaongeza ari ya wanafunzi Kujifunza huku Meneja wa Blue Coast Investment Jeremiah Mussa akisema ukarabati huo umegharimu milioni 43.
Diwani wa Kata ya Mtakuja ambae ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Geita ilipo shule hiyo Costantine Morandi amepongeza hatua hiyo huku Mkurugenzi wa kampuni ya Blue Coast Investment Athanas Inyasi amesema ataendelea kushiriki shughuli za kijamii kwakuwa serikali imeendelea kuweka Mazingira mazuri kwa wawekezaji.
Mkuu wa wilaya ya Geita Cornel Magembe Sambamba nakuipongeza kampuni ya Blue Coast kwa ukarabati huo ameahidi kutoa mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya kuanza ukarabati kwenye Madarasa mengine chakavu yaliyopo kwenye shule hiyo.