Geita mji yapewa siku 30 kukamilisha Zahanati zote zilizotelekezwa
16 November 2023, 12:34 pm
Kutelekezwa kwa Zahanati zaidi ya tatu katika Halmashauri ya mji wa Geita Mkoani Geita kumemuibua Mkuu wa Mkoa nakutoa maagizo kwa watendaji wa serikali katika eneo hilo.
Na Mrisho Sadick – Geita
Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela ametoa mwezi mmoja kwa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya mji wa Geita kuhakikisha anakamilisha Zahanati zote zilizotelekezwa kwa muda mrefu katika halmashauri hiyo.
Shigela akiwa katika ukaguzi wa miradi hiyo ametembelea ujenzi wa zahanati ya Bombambili, Mwatulole na Bwihugule ambazo zimetelekezwa kwa muda mrefu nakuiagiza halmashauri ya mji wa Geita kuhakikisha zinakamilisha ujenzi huo haraka ili wananchi waanze kupata huduma karibu na makazi yao.
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Geita Zahra Michuzi ameahidi kutekeleza agizo hilo kwa muda waliyopewa nakwamba kufiki tarehe 15 mwezi wa kwanza mwaka kesho Zahanati hizo zitakuwa zimekamilika huku meneja Mwandamizi anayeshughuliki mahusiano ya jamii kutoka GGML Gilbert Mworia akisema watashirikiana na halmashauri ya mji kutekeleza agizo hilo.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Geita Cornel Magembe amemuahidi mkuu wa mkoa wa Geita kuwa atasimamia utekelezaji wa miradi hiyo kila hatua ili ikamilike kwa muda uliyopangwa.