Chato Utalii Festival kuvutia wawekezaji
25 October 2023, 11:23 am
Mkakati wa wilaya ya Chato kutangaza fursa za uwekezaji katika sekta ya utalii umeanza kupitia matamasha mbalimbali.
Na Mrisho Sadick:
Wilaya ya Chato imepanga kutumia tamasha la Chato Utalii Festival kuvutia wawekezaji katika sekta ya Utalii kwakuwa wilaya hiyo ina vivutio mbalimbali ikiwemo hifadhi ya Taifa ya Rubondo na Burigi Chato.
Akizungumza na waandishi wa Habari Juu ya tamasha hilo, Mkuu wa wilaya ya Chato Mhe. Deusdedith Katwale amesema litaanza Novemba 26 hadi Disemba 3 mwaka huu katika viwanja vya Magufuli Chato huku tamasha likitawaliwa na matukio mbalimbali ikiwemo Marathon, mpira wa miguu wa mashambiki wa Simba na Yanga wakiongozwa na wasemaji wa vilabu hivyo lengo likiwa nikuvutia wawekezaji.
Nae kamishna msaidizi wa uhifadhi na maendeleo ya biashara Kanda ya magharibi TANAPA Albert Mziray ameahidi kutoa ushirikiano kwa kuhakikisha Chato Utalii Festival inakuwa chachu katika nyanja ya utalii na uwekezaji.
Kwa upande wake Ombeni Hingi Mhifadhi mwandamizi hifadhi ya taifa ya Burigi Chato amesema katika hifadhi hiyo kuna fursa nyingi za uwekezaji ikiwemo ya maradhi , huduma ya chakula na usafirishaji wa wageni huku Mhifadhi mkuu wa hifadhi ya taifa ya Rubondo Imani Kikoti akisema kwasasa hifadhi hiyo ina mazingira bora nakuwaalika wananchi kutembelea kujionea vivutio mbalimbali.
Kwa upande wake Katibu Wa TWCC Mkoa Wa Geita Bi Evalyn Bwire na makamu mwenyekiti wa TCCIA Bertha Komba wametumia fursa hiyo kuwakaribisha wanawake na wajasiriamali wengi kujitokeza katika maonesho hayo kwakuwa yanafursa nyingi.