TCRA: Ni kosa kutumia kitambulisho cha mtu mwingine
19 October 2023, 11:46 am
Bado kuna wimbi kubwa la wananchi ambao wanaendelea kutumia vitambulisho vya taifa vya watu wengine kusajili laini zao za simu jambo ambalo ni kinyume na sheria za nchi.
Na Mrisho Sadick:
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA imetoa onyo kwa watu wanaoendelea kutumia vitambulisho vya taifa vya watu wengine kusajilia laini zao za simu kuwa ni kosa kisheria.
Kauli hiyo imetolewa na Meneja wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA Kanda ya Ziwa Mhandisi Francis Mihayo katika warsha ya siku moja ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari wa mkoa wa Geita wa kufuata na kuondoa ukiukwaji wa sheria, kanuni na maadili ya utangazaji iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela Akizungumza katika Warsha hiyo amesema Ofisi yake haitakuwa kikwazo kwa waandishi wa habari kutekeleza majukumu yao huku afisa habari wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita Boaz Mazigo akiwataka waandishi wa Habari kuendelea kuzingatia sheria za uandishi wa Habari.