Shule ya kwanza yenye kidato cha tano Mbogwe yaanza kupokea wanafunzi
29 August 2023, 11:08 am
Wazazi na walezi wenye wanafunzi wa kidato cha tano waliopangiwa katika shule ya sekondari Mbogwe Mkoani Geita wawaruhusu kwenda shule kwani idadi ya wanafunzi walioripoti ni ndogo.
Na Mrisho Sadick:
Kamati ya siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Geita imewatoa hofu wanafunzi waliyochaguliwa kujiunga kidato cha tano katika shule ya sekondari Mbogwe wilayani Mbogwe ikiwa ndiyo shule ya kwanza katika wilaya hiyo kuwa na kidato cha tano.
Shule ya sekondari mbogwe ilifunguliwa mwaka 2005 kwa wanafuzi wa kutwa wasichana na wavulana huku kwa wanafunzi wa kidato cha tano imefunguliwa mwaka huu kwa kupangiwa wanafunzi 89 katika tahasusi za PCB na HGL na wanafunzi waliyoripoti mpaka sasa ni 24 pekee.
Ikiwa ni mara ya kwanza shule hiyo kupokea wanafunzi wa kidato cha tano Kamati ya siasa ya chama cha mapinduzi CCM Mkoa wa Geita imewatembelea wanafunzi hao kubaini iwapo kuna changamoto zinazowakabili.
Baadhi ya wanafunzi waliyochaguliwa kujiunga katika shule hiyo kutoka maeneo mbalimbali hapa nchini wameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kuboresha elimu huku wakiahidi kufanya vizuri kitaaluma.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita Nicholous Kasendamila amewaondoa hofu wanafunzi hao huku kaimu Mkuu wa Mkoa wa Geita Cornel Magembe akisema serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia katika eneo hilo.