Busanda waomba vituo vya kuchotea maji viongezwe
28 August 2023, 1:52 pm
Serikali kupitia wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini RUWASA imeendelea kusogeza huduma hiyo hadi maeneo ya vijijini ambayo yalikuwa yakikabiliwa na changamoto ya maji safi.
Na Mrisho Sadick:
Wakazi wa kijiji cha Busanda wilayani Geita wameiomba serikali kuwaongezea vituo vya kuchotea maji baada ya kukamilika kwa mradi wa maji uliyojengwa kwa thamani ya zaidi ya shilingi milioni 200 utakao hudumia watu zaidi ya elfu sita katika eneo hilo.
Wakizungumza mbele ya kamati ya siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Geita iliyotembelea nakukagua maendeleo ya mradi huo, baadhi ya wakazi wa kijiji hicho wamesema kabla ya mradi huo kutekelezwa walikuwa wakichangia maji na wanyama pamoja na kusumbuliwa na maradhi ya tumbo.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kaimu meneja wa RUWASA wilaya ya Geita Pius Didackus amesema chanzo cha maji cha mradi huo nikisima cha kina kirefu chenye uwezo wa kuzalisha maji lita elfu 65 kwa saa.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita Nicholous Kasendamila akiwataka wananchi kuulinda mradi huo ili utumike kwa muda mrefu huku kaimu mkuu wa Mkoa wa Geita Cornel Magembe amesema serikali itahakikisha inafikisha huduma za maji na umeme katika taasisi zote za umma Mkoani Geita.
Kamati hiyo ikiwa katika halmashauri ya mji wa Geita imeridhishwa na utekelezaji mzuri wa ujenzi wa shule za msingi na sekondari nakuwataka watendaji wa serikali kuendelea kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha za miradi.