Ubovu wa barabara wawaibua wananchi Ikunguigazi Geita
17 August 2023, 1:12 pm
Kuelekea msimu mpya wa mvua wananchi wilayani Mbogwe wamezihofia barabara zao zikiwemo zilizotelekezwa kwa muda mrefu huenda zikawapa changamoto iwapo hazitafanyiwa marekebisho.
Na Nicholous Lyankando:
Wananchi wa vijiji vya Ikunguigazi na Nyikonga wilayani Mbogwe mkoani Geita wamesikitishwa na kitendo cha barabara inayounganisha vijiji hivyo kutelekezwa zaidi ya miaka 5 bila kutengenezewa kivuko.
Wakizungumzia adha hiyo baadhi ya wananchi wamesema barabara hiyo kwa sasa haitumiki kwa muda mrefu na ni kunganishi kikubwa kwa vijiji hivyo kiuchumi lakini badala yake imegeuka kama mapitio ya wanyama baada ya kivuko chake kukatika.
Viongozi wa serikali ya vijiji hivyo akiwemo mwenyekiti wa kijiji cha Ikunguigazi Jumanne Richard wamesema barabara hiyo miaka ya nyuma wakati inatumika ilikuwa kiunganishi muhimu kiuchumi kati ya vijiji hivyo na tayari kunajitihada kwajili ya kuifufua.
Kaimu meneja wa wakala wa barabara za mijini na vijijini TARURA wilaya ya mbogwe George reuben alisema barabara nyingi wameshaziweka katika mpango wa fedha wa mwaka huu ili zikarabatiwa na akawatoa wasiwasi wananchi.