Zaidi ya milioni 150 zatumika ujenzi bweni la wanafunzi wenye mahitaji maalum Katoro
24 July 2023, 1:38 pm
Wanafunzi wenye mahitaji maalum katika shule ya msingi Katoro wilayani Geita wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwajengea bweni ambalo limegharimu kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 150.
Serikali imeendelea kuboresha mazingira kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu kwa kujenga miundombinu rafiki ya elimu ili kuwa kichocheo cha wazazi na walezi kuwapeleka shule watoto wa aina hiyo.
Na Mrisho Sadick:
Wametoa shukrani hizo kwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan baada ya kutembelewa na kamati ya utekelezaji ya jumuia ya wazazi ya CCM Kata ya katoro wilayani Geita iliyofika kuona maendeleo ya bweni hilo.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya msingi katoro Jeremia Kishiga amesema bweni hilo linauwezo wa kubeba wanafunzi 80 na kitengo hicho kina wanafunzi 116, wakike 46 na wakiume 70 na fedha za ujenzi wa bweni hilo zimetoka serikali kuu huku milioni 45 ni mapato ya ndani ya halmashauri ya wilaya ya Geita.
amesema licha ya serikali kuwajengea bweni hilo lakini wanakabiliwa na changamoto ya vitanda kwakuwa wana idadi kubwa ya wanafunzi ambao hawana vitanda nakuiomba serikali kuwasaidia.
Wajumbe wa kamati hiyo wamewataka wazazi na walezi wenye watoto wenye mahitaji maalumu kutowaficha huku mwenyekiti wa kamati hiyo Deusdedit Nzenzule akiipongeza serikali kwa kuonesha nia ya kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalumu katika shule hiyo.