Huduma usafiri wa dharura kwa wajawazito yazinduliwa Geita
3 July 2023, 12:23 pm
Tatizo la vifo vya wanawake wajawazito na watoto mkoani Geita bado ni kubwa na kutokana na changamoto hiyo serikali imekuja na njia mbadala ya kupunguza tatizo hilo.
Na Mrisho Sadick – Geita
Serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 218 kwa ajili ya usafirishaji wa dharura kwa akina mama wajawazito na watoto wachanga mkoani Geita.
Hayo yamebainishwa na mganga mkuu wa mkoa wa Geita Dkt. Omari Sukari wakati wa uzinduzi wa programu ya M-MAMA kwa ajili ya kuimarisha utoaji wa huduma za afya kwa akina mama wajawazito na watoto wachanga na kwamba mpaka sasa wamesajili magari binafsi 79 yatakayotumika kuwabeba huku mratibu wa mfumo huo kutoka taasisi ya PATHFINDER URIEL KINUMA akisema madereva hao watakuwa wakilipwa shiligi 1,300 kwa kilometa.
Zoezi hilo limefanyika hosptali ya rufaa ya mkoa wa Geita ambapo mwakilishi wa katibu tawala wa mkoa wa Geita Herman Matemu na mkurugenzi mkuu wa taasisi ya TATHMINI UHAI Banzi Msumi wamesema hatua hiyo itasaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto kwa kuwa tatizo hilo Geita ni kubwa.
Mkuu wa mkoa wa Geita Martine Shigela amesema licha ya kuwepo kwa program hiyo amesisitiza akina mama wajawazito kuendelea kuhamasishwa kuhudhuria kliniki huku baadhi ya wananchi wa mkoa wa Geita Chamila Frank na Neema Nela wakiishukuru serikali kwa mpango huo.