Tamasha la utalii Chato fursa kwa wakazi wa Geita.
10 August 2021, 2:57 pm
Na Mrisho Sadick:
Wananchi Mkoani Geita wameshauriwa kutumia fursa ya maonesho ya utalii yanayoendelea wilayani Chato kwa kufika nakuonesha bidhaa zao za kiasili ikiwa ni njia mojawapo ya kujitangaza nakufahamika zaidi.
Maonesho hayo yalianza kwa Waendesha mitumbwi 87 kutoka kwenye mialo mbalimbali katika eneo la Ziwa Victoria wilayani Chato mkoani Geita kushiriki mashindano ya kupiga makasia lengo likiwa ni kuhamasisha utalii kwenye hifadhi ya kisiwa cha Rubondo.
Mbio za mashindano hayo zimeanza kwenye hifadhi ya Rubondo na kuishia eneo la Mwelani kata ya Mganza umbali wa kilomita nane.
Wakizungumza mara baada ya kuhitimisha mashindano hayo baadhi ya washiriki wameomba mashindano hayo yawe ya mara kwa mara ili kujenga mahusiano mazuri baina yao na wahifadhi wa kisiwa cha Rubondo kilichopo katika wilaya ya Chato.
Mkuu wa wilaya ya Chato, Martha Mkupasi akizungumza na washiriki amesema mashindano hayo ni kutangaza utalii katika hifadhi ya Rubondo na Chato kwa ujumla nakuwashauri wananchi katika eneo hilo na maeneo jirani kuendelea kujitokeza kwa wingi kuchangamkia fursa hiyo.
Amewataka wapiga makasia kujenga ushirikiano baina yao na watumishi wa Rubondo pamoja na kulinda uvuvi katika Ziwa Victoria na kuachana na uvuvi haramu kwenye eneo la hifadhi.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemery Senyamule, mkuu wa wilaya ya Geita, Mhe , Wilson Shimo amewashauri wapiga makasia hao kuendelea kutangaza utalii wa kisiwa cha Rubondo kwa manufaa ya wilaya ya Chato na Taifa la Tanzania.
Wananchi kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya Mkoa wa Geita wanaendelea kujitokeza kwenye tamasha la utalii na maonyesho ya biashara yaliyoanza Agosti 7 hadi 15, 2021 yamekua na mvuto wa aina yake.