Uchimbaji holela wa madini ya dhahabu waathiri Maeneo ya kilimo na makazi
31 May 2021, 2:00 pm
WAKAZI wa vijiji vya Lwamgasa wilayani Geita na Nampalahala wilayani Bukombe Mkoani Geita vinavyopakana na mapori ya hifadhi wameiomba Serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania kuwaruhusu kutumia baadhi ya maeneo hayo kwa shughuli za kilimo na makazi kutokana na ongezeko la watu katika vijiji hivyo.
Wakizungumza na Storm FM kwa nyakati tofauti baadhi ya wakazi wa kijiji cha Lwamgsa wamesema eneo kubwa katika kijiji hicho limeathiriwa na shughuli za uchimbaji wa madini ya dhahabu hivyo kukosa maeneo ya kilimo na makazi kutokana na ongezeko la idadi ya watu kijijini humo.
Kwa upande wao baadhi ya wakazi wa kijiji cha Nampalahala wilayani Bukombe wameiomba serikali kupitia kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe, Samia Suluhu kuwapatia kipande cha aridhi kutoka katika pori la hifadhi la eneo hilo kwa ajili ya shughuli za kilimo.
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Lwamgasa Bw Mussa Songoma na Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Nampalahala Bw Peter Magadula wamesema kuna haja ya serikali kuwasaidia wananchi kwa kuwapatia aridhi kwa ajili ya shughuli za kilimo kwakuwa maeneo mengi yameathiriwa na shughuli za uchimbaji wa madini ya dhahabu.