Mashabiki wote watakuwa salama katika Mchezo wetu na Pamba FC
16 April 2021, 11:13 pm
Mjumbe wa kamati kuu tendaji wa chama cha mpira wa miguu Geita (GEREFA) Simon Shija amesema kila kitu kwa maana ya maandalizi kuelekea mchezo wa kesho ligi daraja la kwanza Tanzaniabara baina ya Geita Gold FC dhidi ya Pamba SC yamekamilika hivyo mashabiki wasiwe na wasiswasi.
Shija amesema tayari ofisa kutoka TFF ameshawasili kwa ajili ya kuratibu mchezo huo na wao kama chama cha mpira wa miguu mkoa wameshaandaa mazingira rafiki kuanzia uuzwaji wa tiketi ,ulinzi pamoja na utaratibu wa kuingia mashabiki uwanjani ili kuwawezesha mashabiki kupata fursa ya kuushuhudia mchezo huo.
Nae mjumbe wa hamasa wa Geita Gold FC Gabriel Nyasiru ameendelea kuwasisitiza mashabiki wa Geita Gold kuwahi mapema kwenye uwanja wa Nyankumbu ili kuepusha msongamano wa mashabiki kwani kuanzia saa 2:00 asubuhi lango la uwanja huo litakuwa wazi huku msemaji wa timu hiyo Aman Nicholaus amesema tiketi zipo za kutosha nakwamba wakazi wa Geita na viunga vyake wajitokeze kwa wingi kuipa nguvu timu yao.
Mchezo huo wa raundi ya 12 utapigwa kwenye dimba la shule ya wasichana ya Nyankumbu kuanzia majira ya saa 10:00 alasiri ukiwakutanisha vinara Pamba FC wenye alama 27 dhidi ya Geita Gold FC wanaoshik nafasi ya pili na alama 25.