Waganga na wakunga wa tiba asili Tanzania wamlilia Dkt. Magufuli
24 March 2021, 6:45 pm
Na Mrisho Sadick – Geita
Siku chache baada ya kufariki aliekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, Umoja wa waganga na wakuga wa tiba asili Tanzania (UWAWATA) umesema kufariki kwa kiongozi huyo ameacha pengo kubwa kwa upande wao kwa kile walichokieleza kuwa alipanga kuboresha huduma hiyo kwa miaka mitano ya awamu ya pili ya uongozi wake.
Wakizungumza na kipindi hiki katika maeneo yao ya kazi Mkoani Geita baadhi ya waganga na wakunga wa tiba asili katika eneo hilo wamese utawala wa Dkt Magufuli ulilenga kuimarisha tiba asili kwakuwa imekuwa na mchango mkubwa kwa taifa.
Bugota Bujukano ni Mganga wa Tiba asili kutoka Mkoani Simiyu amelazimika kutembea kwa miguu kutoka Simiyu hadi Geita kwa lengo la kwenda kushiriki mazishi ya Dkt Magufuli wilayani Chato.
Mwenyekiti wa umoja huo akiwa mkoani Geita Bujukano Mahungu Jonh amesema kwa niaba ya umoja huo anatoa pole kwa watanzania wote na familia ya Dkt Magufuli huku akisema katika uhai wake aliipa kipaumbele tiba asili kuliko tawala zingine zilizopita huku akimuomba Mhe, Samia Suluhu aliekabidhiwa kijiti hicho kufuata nyayo zake ili kuboresha huduma hiyo itakayo saidia kupunguza changamoto ya matibabu hususani maeneo ya vijijini.
Akifungua Bunge la 12 la jamhuri ya muungano wa Tanzania Novemba 13 mwaka 2020 Dkt Magufuli alisema katika miaka mitano ya uongozi wake alikusudia kuimarisha kitengo cha utafiti wa tiba mbadala sambamba na kuruhusu matibabu na maduka ya kuuza dawa za tiba asili.