Afariki dunia kwa kusombwa na maji akitoka kunywa pombe.
3 January 2023, 9:06 am
Na Mrisho Sadick:
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Mkoani Geita wamefanikiwa kuupata mwili wa Matunda Nyama mwenye umri wa miaka (61) Mkazi wa Kata ya Buhalahala halmashauri ya mji wa Geita aliyesombwa na maji siku mbili zilizopita wakati akitoka kunywa pombe za kienyeji Kijiji jirani.
Balozi wa Mtaa huo Dominick Songoma amesema siku mbili zilizopita marehemu hakuonekana nyumbani kwake ndipo walipoanza kumtafuta, nakwamba taarifa za awali ilisemekana kuwa alikwenda kijiji jirani kunywa pombe za kienyeji wakati anarudi alishindwa kuvuka mto nakusombwa na maji.
Mkuu wa Kitengo cha oparesheni kutoka Jeshi la zimamoto na uokoaji Mkoani Geita Sanjeti Evodius Komba amewasisitiza wananchi kuendelea kuchukua tahadhari katika kipindi hiki cha mvua ili kuepukana na matukio ya watu kufa maji.
Siku tatu zilizopita katika Halmashauri hiyo lilitokea tukio la mtu kufariki dunia kwa kusombwa na maji wakati akijaribu kuvuka kwenda upande wa pili.