Wadaiwa kuvamia makazi ya watu na kuanza uchimbaji wa madini
10 May 2024, 5:30 pm
Mkoa wa Geita ni miongoni mwa mikoa inayojihusisha na uchimbaji mdogo, wa kati na mkubwa wa madini ya dhahabu. Licha ya mazingira kuboreshwa ili kufanikisha shughuli za uchimbaji bado kuna changamoto ya baadhi ya watu kuvamia makazi ya watu na kuendesha shughuli za uchimbaji.
Wakazi wa mtaa wa Katoma kata ya Kalangalala halmashauri ya mji Geita wameiomba serikali kuingilia kati suala la baadhi ya watu wanaodaiwa kuendesha shughuli za uchimbaji katika makazi yao wakihofia nyumba zao kuanguka kutokana na shughuli hizo.
Wakizungumza na Storm fm, baadhi ya wananchi wanaoishi karibu na eneo hilo wamesema shughuli zinazoendelea zinawaathiri kwa kiasi kikubwa kwani kuna baadhi ya mabomba ya maji yamekatwa na kusababisha kukosa huduma ya maji kwa muda sasa.
Mwenyekiti wa mtaa huo Evarist Kaitana amekiri kupokea taarifa hiyo na ofisi yake inaendelea kufuatilia ukweli zaidi wa jambo hilo.
Akizungumza kwa njia ya simu Afisa madini mkoa wa Geita Samwel Shoo amesema shughuli inayoendelea katika eneo hilo ni ujenzi na siyo uchimbaji kama wananchi wanavyodai licha ya eneo hilo kuonekana lina mchanga unaosadikika kuwa na madini ya dhahabu.
Mamlaka ya mazingira Halmashauri ya mji Geita wameahidi kufika eneo la tukio na kuangalia athari zipo kwa kiasi gani.