Walimu walia na uhaba wa nyumba za watumishi kata ya Nyamalimbe
2 May 2024, 3:52 pm
Siku ya wafanyakazi duniani ambayo huadhimishwa kila mei mosi ya kila mwaka huangazia mafanikio na haki za wafanyakazi kwa kufanya maandamano, mikutano na matukio mengine yakiambatana na mashinikizo ya kutambua haki za wafanyakazi.
Na: Edga Rwenduru – Geita
Baadhi ya walimu kata ya Nyamalimbe iliyopo halmashauri ya wilaya ya Geita wameeleza changamoto ya kuishi mbali na vituo vyao vya kazi kutokana na shule wanazofanyia kazi kutokuwa na nyumba za watumishi jambo ambalo linawalazimu kuingia gharama za usafiri.
Wakizungumza katika maadhimisho ya mei mosi katika kata hiyo ambayo yamefanyika katika shule ya sekondari Nyamalimbe Laurent Salveston na Tatu Hamis ambao ni walimu wameiomba serikali kuwajengea nyumba za watumishi.
Diwani wa kata ya Nyamalimbe Jeremiah Ikangara pamoja na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Geita Nicolaus Kasendamila wamekiri kuwepo kwa changamoto hiyo huku wakisema tayari mpango wa ujenzi wa nyumba hizo kila shule umeanza.
Akiwa katika maadhimisho ya mei mosi kimkoa yaliyofanyika wilayani Mbogwe, Mkuu wa mkoa wa Geita Martine Shigela ambaye alikuwa mgeni rasmi amesema serikali inafanya jitihada za kutatua changamoto zote za watumishi.