Washiriki 400 waanza maonesho katika viwanja vya EPZA Geita
21 September 2023, 5:33 pm
Washiriki kutoka mataifa mbalimbali kama vile China, Rwanda, Burundi na mengineyo yameshiriki maonesho hayo ya 6 yaliyoanza rasmi mwaka 2018.
Na Zubeda Handrish- Geita
Mkuu wa Mkoa wa Geita Martin Shigela amesema kuwa maonesho ya dhahabu ambayo yameanza jana Septemba 20, 2023 katika viwanja vya EPZA mjini Geita yameanza kwa mwitikio mkubwa wa washiriki ikilinganishwa na mwaka jana.
Ameyaema hayo leo Septemba 21, 2023 katika viwanja vya EPZA na kuongeza kuwa hadi kufikia leo washiriki 400 kutoka ndani na nje ya nchi wamefika katika maonesho ikiwa ni idadi kubwa ya washiriki ukilinganisha na washiriki 250 wa mwaka jana.
Amesema kuwa maonyesho hayo yatazinduliwa rasmi na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dr. Doto Biteko Septemba 23 mwaka huu na yatafungwa rasmi na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mhe. Samia Suluhu Hassan Septamba 30, mwaka huu.
Maonesho ya 6 ya kimataifa ya teknolojia ya madini 2023, yamebeba kaulimbiu isemayo “matumizi ya teknolojia sahihi katika kuinua wachimbaji wadogo kiuchumi na kuhifadhi mazingira”.