Serikali yavuna zaidi ya bilioni 118 soko kuu la dhahabu Geita
1 September 2023, 4:51 pm
Kuanza kutumika kwa kanuni za masoko ya madini za mwaka 2019 chini ya sheria ya madini sura ya 123 zimekuwa na manufaa makubwa kwa serikali na Wananchi wanaofanya shughuli za uchimbaji wa madini ya Dhahabu Mkoani Geita.
Na Mrisho Sadick:
Mkoa wa Geita ni miongoni mwa Mikoa inayozalisha madini ya dhahabu kwa wingi na tangu kuanzishwa kwa soko Kuu la dhahabu Geita mwaka 2019 serikali kupitia tume ya madini imekusanya tozo ya mrabaha na ada ya ukaguzi zaidi ya Bilioni 118.
Akizungumza mbele ya Wahariri wa vyombo vya Habari waliyopo Mkoani Geita kwa ziara ya siku tatu ya kutembelea nakujione fursa mbalimbali za kiuchumi ,mwakilishi wa Afisa madini Mkazi Geita Hussein Nzima amesema mbali na uwepo wa soko Kuu na masoko madogo madogo ya madini ya dhahabu ofisi ya afisa madini mkazi Geita imekusudia kukusanya bilioni 240 katika mwaka wa fedha 2023/2024.
Wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu Mkoani Geita Nassoro Salum na Ester Maduhu wameipongeza serikali kwa kuendelea kutatua changamoto zinazowakabili ikiwemo kuwapeleka katika mataifa ya nje kupata ujuzi wa uchimbaji salama na wenye tija.
Baadhi ya Wahariri wa vyombo vya Habari akiwemo Basil Elias wa ITV na Adela Atilia wa Wasafi TV wametumia ziara hiyo kuishauri serikali kuwekeza katika teknolojia na kuwakopesha vifaa vya kisasa wachimbaji wadogo kwakuwa wanatumia zana duni katika shughuli zao.
Wahariri hao wametembelea katika mradi wa umwagiliaji wa Ibanda Igaka,Soko Kuu la madini Geita,Mgodi wa Buckreef , Mgodi wa uchimbaji Mdogo wa Nassoro Kisha wakahitimisha Katika Mgodi wa Mfano wa Lwamgasa, ziara hiyo ikiwa ni maandalizi ya Kuelekea maonesho ya sita ya kitaifa ya madini Mkoani Geita ambayo yanatarajia kufanyika kuanzia septemba 20 mwaka huu.