Moto uliyozuka eneo la uwekezaji wadhibitiwa
12 July 2023, 11:32 am
Wananchi Mkoani Geita wametakiwa kutoa taarifa haraka pindi wanapohitaji msaada wa maokozi kutoka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ili kukabiliana na tatizo kabla halijawa kubwa.
Na Mrisho Sadick:
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoani Geita limefanikiwa kuudhibiti moto uliyozuka karibu na Jengo la Ofisi za uwekezaji EPZA katika Kata ya Bombambili Halmashauri ya mji wa Geita Mkoani Geita.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na uokoaji Mkoani Geita Inspekta Edward Lukuba amesema tukio hilo limetokea majira ya saa sita mchana baada ya kupata taarifa kutoka kwa wananchi nakwamba uchunguzi zaidi unaendelea ili kubaini chanzo cha moto huo na hakuna madhara ya kibinadamu yaliyotokea.
Baadhi ya Wananchi walioshuhudia tukio hilo wamesifu ufanisi wa Jeshi la Zimamoto na uokoaji Mkoani Geita kwa kufika kwa wakati nakuudhibiti moto huo kwani ungeleta athari kwenye miundombinu ya umeme na vibanda vilivyo katika eneo hilo.
Katika Hatua nyingine Inspekta Lukuba amewataka Wananchi kuendelea kutoa taarifa mapema pindi wanaohitaji msaada wa maokozi kwa kupiga simu ya bure ya 114.