Storm FM

Kijana mwenye ulemavu apatiwa baiskeli Geita

28/02/2026, 16:42

MNEC Evarist Gervas akiwa na baadhi ya viongozi wa chama na kata ya Kasamwa pamoja na kijana Zabron baada ya kukabidhiwa kiti mwendo. Picha na Mwandishi wetu

“Naimani baiskeli hii itamsaidia kuweza kutimiza majukumu yake ya kila siku naimani pia ataitunza vizuri” – MNEC Evarist Gervas

Na: Ester Mabula

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa kutoka mkoa wa Geita, Evarist Gervas, ametimiza ahadi yake ya kumpatia baiskeli kijana mwenye ulemavu anayefahamika kwa jina la Zabron Juma Manyasima, mkazi wa Kasamwa, kata ya Kasamwa, wilaya ya Geita mkoani Geita.

Ahadi hiyo aliitoa Februari 25, 2025, na sasa imetekelezwa rasmi baada ya kukabidhi baiskeli hiyo nyumbani kwa kijana huyo.

Zabron Juma, kijana mwenye ulemavu aliyekabidhiwa kiti mwendo na MNEC Evarist Gervas. Picha na Mwandishi wetu

Katika hafla hiyo ya makabidhiano, MNEC Evarist Gervas aliambatana na wajumbe wa kamati ya siasa ya Kata pamoja na Diwani wa Kata ya Kasamwa Bi Mary Kasanda.

Akizungumza baada ya makabidhiano hayo, Evarist Gervas amesema kuwa hupata furaha kwa kusaidia wengine, na ameonesha kuridhishwa kwake kwa kufanikisha kumpatia Zabroni baiskeli hiyo akieleza kuwa ana imani kijana huyo ataitunza na kuitumia ipasavyo ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Kasamwa Marry Kasanda amemshukuru MNEC huyo kwa kutimiza ahadi yake, akisema kuwa msaada huo utamsaidia kwa kiasi kikubwa kijana huyo katika shughuli zake na kumrahisishia maisha yake ya kila siku.