Storm FM
Storm FM
16 February 2026, 11:44 pm

Ni mwendelezo wa ziara za diwani wa kata ya Kalangalala kutembelea maeneo mbalimbali kwa lengo la kusikiliza kero za wananchi na kuweza kuzitatua.
Na: Ester Mabula
Wananchi wakazi wa mtaa wa Nyanza, kata ya Kalangalala, halmashauri ya manispaa ya Geita mkoani Geita wametoa malalamiko juu ya mwekezaji ambaye ni kampuni ya Lespio Gold Mine inayojihusisha na uchimbaji mdogo wa madini ya dhahabu katika eneo hilo.
Malalamiko hayo wameyatoa mbele ya diwani wa kata hiyo Reuben Sagayika katika mkutano wa hadhara uliofanyika leo Februari 16, 2026 katika mtaa huo wakieleza kuwa shughuli zinazofanyika hapo zimekuwa zikileta usumbufu mkubwa kwani kazi hufanyika usiku na mchana.

Akizungumzia sakata hilo, Mhandisi wa migodi kutoka ofisi ya RMO mkoa wa Geita Bw. John Ayoub ameeleza kuwa kwa sasa shuhuli za upasuaji miamba zisitishwe hadi pale taratibu zitakapofanyika upya za kufanya tathmini sambamba na ulipwaji wa fidia kwa wananchi hao.

Akizungumza meneja wa kampuni hiyo Bw. Soud Mtafuni amesema amepokea maelekezo yaliyotolewa na serikali na kueleza kuwa hatua za kulipa fidia zimekwisha anza hivyo zitafanyika haraka ili kuweza kuendelea na shughuli hiyo pasipo kuathiri wananchi.
Diwani wa kata ya Kalangalala Reuben Sagayika amewataka wananchi kuwa watulivu huku akieleza suala hilo litatatuliwa kwa kuzingatia maslahi ya pande zote mbili.
