Storm FM
Storm FM
1 February 2026, 2:01 pm

Mgodi wa GGML uliopo mkoani Geita umeendelea kuwa chachu ya maendeleo nchini kupitia ushirikiano wake na serikali katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo kupitia Afya, Elimu, Miundombinu nk
Na: Ester Mabula
Naibu Waziri wa madini Dkt. Steven Kiruswa amesema sekta ya madini kwa mwaka 2024 imechangia asilimia 10.1 kwenye pato la taifa, akisema mchango huo ni zaidi ya malengo waliyojiwekea katika kipindi hicho na kuchangiwa na wadau mbalimbali ukiwemo mgodi wa Geita Gold Mining Limited (GGML).
Dkt. Kiruswa amesema hayo kwenye hafla ya maadhimisho ya miaka 25 ya uwepo wa kampuni ya uchimbaji madini nchini GEITA GOLD MINING LIMITED (GGML) iliyopo mkoani Geita akisema mafanikio hayo yametokana na mabadiliko ya sheria mbalimbali za madini pamoja na ushirikiano wa wawekezaji wa sekta hiyo.

Kwa upande GGML, akizungumza Makamu wa Rais wa AngloGold Ashanti wa masuala ya uendelevu na mambo ya ubia Afrika Bw. Simon Shayo amesema kupitia uchimbaji wa dhahabu imeweza kubadilisha maisha ya wakazi wa mkoa huo kupitia miradi mbalimbali ya kijamii ambapo wamechangia zaidi ya shilingi Bilioni 52 kwenye miradi hiyo.
Katika kipindi cha miaka 25, GEITA GOLD MINING LIMITED imefanikiwa kusaidia maendeleo mbalimbali ya kiuchumi, ikiwemo kulipa kodi ya dola za marekani Bilioni tatu kwa serikali ya Tanzania, huku ikifanikiwa kutoa mamilioni ya ajira kwa watanzania.
