Storm FM

Halmashauri ya Manispaa ya Geita yapata viongozi wapya

2 December 2025, 3:50 pm

Mwenyekiti wa uchaguzi wa viongozi wa halmshauri ya manispaa ya Geita Bi. Lucy Beda. Picha na Ester Mabula

Leo Disemba 02, 2025 kikao cha kwanza cha baraza la madiwani kimefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Dkt. Samia Suluhu Hassan eneo la Bombambili manispaa ya Geita.

Na: Ester Mabula

Baraza la madiwani la halmashauri ya manispaa ya Geita limeketi leo Disemba 02, 2025 na kufanya uchaguzi wa viongozi wapya watakaoongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, ambao ni Mstahiki Meya na Naibu Meya.

Agenda za mkutano wa kwanza wa uzinduzi wa baraza la madiwani manispaa ya Geita ni pamoja na viapo vya madiwani, viapo vya maadili na kujaza tamko la mali na madeni kwa viongozi, uchaguzi wa mstahiki Meya na Naibu Meya pamoja na kuunda kamati za kudumu katika idara mbalimbali.

Baadhi ya madiwani wakiwa katika kikao cha Baraza kilichoketi leo Disemba 02. Picha na Ester Mabula

Kupitia mkutano huo, Diwani wa kata ya Bombambili, Leonard Bugomola, amechaguliwa kuwa Meya wa Manispaa ya Geita, huku Diwani wa Nyanguku, Elias Ngole, akichaguliwa kuwa Naibu Meya.

Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo Mwenyekiti wa Uchaguzi Bi. Lucy Beda ameeleza kuwa viongozi hao wawili wamechaguliwa kwa kura zote za ndio.

Sauti ya mwenyekiti wa uchaguzi Bi. Lucy Beda

Mara baada ya kuchaguliwa Mstahiki Meya Lenard Bugomola na Naibu Meya Elias Ngole wametoa shukrani zao kwa madiwani sambamba na kueleza vipaumbele vyao katika miaka mitano ijayo.

Sauti ya Mstahiki Meya pamoja na Naibu Meya
Mstahiki Meya Leonard Bugomola akizungumza katika kikao cha Baraza la madiwani. Picha na Ester Mabula