Storm FM

Geita ulinzi umeimarishwa kuelekea uchaguzi

23 October 2025, 7:38 pm

Kamanda wa polisi mkoa wa Geita akizungumzia hali ya usalama kuelekea uchaguzi mkuu. Picha na Kale Chongela

Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita limeendelea kutoa wito kwa wananchi wote kuendelea kudumisha amani, umoja na mshikamano.

Na Kale Chongela- Geita

Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita limewahakikishia wananchi kuwa maandalizi ya ulinzi na usalama yamekamilika kwa kiwango cha juu kuelekea siku ya kupiga kura itakayofanyika Jumatano Oktoba 29 mwaka huu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Safia Jongo ameeleza kuwa ulinzi umeimarishwa kwa asilimia mia moja katika maeneo yote ya Mkoa wa Geita ili kuhakikisha wananchi wanashiriki uchaguzi kwa amani utulivu na usalama wa hali ya juu.

Amesema Jeshi la Polisi limeweka mikakati thabiti ya kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata fursa ya kupiga kura kwa uhuru na bila hofu huku likidhibiti viashiria vyote vya uvunjifu wa amani katika kipindi chote cha uchaguzi.

Kamanda wa polisi mkoa wa Geita akizungumzia hali ya usalama kuelekea uchaguzi mkuu. Picha na Kale Chongela

Aidha Kamanda Jongo amewataka wananchi kuzingatia sheria kanuni na taratibu za uchaguzi kwa kuhakikisha wanabaki mbali na vituo vya kupigia kura mara baada ya kumaliza kupiga kura, ili kutoa nafasi kwa wengine kutekeleza haki yao kwa utulivu.

Sauti ya Kamanda Jongo

Baadhi ya wananchi wa Mkoa wa Geita wamepongeza jitihada za Jeshi la Polisi katika kuimarisha ulinzi wakibainisha kuwa hatua hiyo imeongeza imani na utulivu kuelekea siku ya kupiga kura ,wameeleza kuwa hali ya usalama iliyopo kwa sasa inatoa matumaini ya kufanyika kwa uchaguzi huru, wa haki na wenye amani.

Sauti ya wananchi

Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita limeendelea kutoa wito kwa wananchi wote kuendelea kudumisha amani, umoja na mshikamano, likisisitiza kuwa lipo imara kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa utulivu na kwamba hatua kali zitachukuliwa dhidi ya mtu yeyote atakayehatarisha usalama wa wananchi au kuvuruga mchakato wa uchaguzi.