Storm FM
Storm FM
27 September 2025, 12:42 am







“Ilani ya CCM kwa mwaka 2025 imeainisha maeneo muhimu yanayogusa maisha ya wananchi kwenye afya, elimu, miundombinu pamoja na biashara” – Mhandisi Chacha
Na:Ester Mabula
Mgombea ubunge wa Jimbo la Geita mjini kupitia tiketi ya CCM Mhandisi Chacha Wambura katika mwendelezo wa kampeni zake leo Septemba 26, 2025 ametembelea soko la Nyankumbu ambapo amesikiliza kero na changamoto mbalimbali zinazowakabili katika shughuli zao za kila siku.
Miongoni mwa changamoto zilizotajwa na wajasiriamali wa soko hilo ni pamoja na ukosefu wa maji ya kutosha kwenye vyoo vya soko, kutokuwepo kwa eneo maalum la kushushia mizigo, tatizo la mitaro ya maji, pamoja na malalamiko juu ya tozo za vizimba.
Chacha amewahakikishia wajasiriamali hao kuwa CCM imeweka kipaumbele kikubwa katika kuhakikisha masoko yote nchini yanakuwa na mazingira rafiki kwa wafanyabiashara ili waweze kufanya shughuli zao kwa usalama na tija.
Ameahidi kwamba, akipewa ridhaa ya kuwa Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini, atashirikiana kwa karibu na viongozi wa serikali na taasisi husika kuhakikisha changamoto hizo zinatafutiwa majibu ya kudumu na soko la Nyankumbu linajengwa kwa viwango bora kulingana na mipango ya serikali.
Aidha, Eng. Chacha Mwita Wambura amewaomba wafanyabiashara wa Nyankumbu na wananchi wa Geita kwa ujumla kumpa kura katika uchaguzi mkuu ujao ili aweze kushirikiana nao kwa vitendo katika kuimarisha biashara zao na kuendeleza maendeleo ya Geita.