Storm FM
Storm FM
22 September 2025, 11:37 pm

Septemba 22, 2025 Waziri mkuu wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania mhe. Kassim Majaliwa amezindua rasmi maonesho ya 8 ya teknolojia na uwekezaji katika sekta ya madini yanayofanyika katika viwanja vya Dkt. Samia Suluhu manispaa ya Geita.
Na: Ester Mabula
Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imesema inajivunia kuendelea kushirikiana na serikali katika kuandaa maonesho ya kitaifa ya teknolojia ya madini hapa nchini ambayo yameendelea kukua siku hadi siku na kuonesha namna sekta hiyo inavyoinufaisha Tanzania.
Akiongea wakati wa ufunguzi wa maonesho ya 8 ya kitaifa ya teknolojia ya madini, makamu wa Rais wa masuala ya uendelevu wa AngloGold Ashanti inayomiliki mgodi wa GGML, Bw. Simon Shayo amesema kuwa mgodi huo unajivunia miaka 25 ya uwepo wake hapa nchini, ukiwa sio tu kwa ajili ya uwekezaji, bali kama mdau wa maendeleo ya jamii.

“Tunajivunia mafanikio mbalimbali tuliyoyapata, ikiwemo kutoa mchango mkubwa wa maendeleo na ajira kwa Watanzania, tumeajiri zaidi ya watu 7,000, ambapo asilimia 98 ya watu hao ni Watanzania, na asilimia 88 ya idadi hiyo wanashiriki katika ngazi za usimamizi wa kampuni (management) na maamuzi,” amesema Bw. Simon, na kuongeza
“Lakini pia tumekeleza miradi mingi ya maendeleo ndani ya mkoa wa Geita kwa kushirikiana na jamii na Serikali katika kuboresha sekta mbalimbali ikiwemo maji, afya elimu na miundombinu ya barabara,” amesema.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela amesema kuwa mgodi huo umekuwa mdau mkubwa wa maendeleo, ukichangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa haraka wa mkoa huo kupitia uwekezaji wake.

Awali, wakati akifungua maonesho hayo, Waziri mkuu wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amesema kuwa sekta hiyo kupitia wadau mbalimbali ikiwemo GGML imekuwa ikikua kwa kasi na kuchangia asilimia 10.1 ya Pato la Taifa (DGP) mwaka 2024.