Storm FM
Storm FM
20 September 2025, 8:37 pm

Serikali imenunua mitambo 15 kwa ajili ya wachimbaji wadogo na itaendelea kuwaunga mkono kila hatua
Na Mrisho Sadick:
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa leseni 17 na vifaa vya kisasa vya uchimbaji wa madini ya dhahabu kwa vikundi vya wanawake wanaofanya shughuli za uchimbaji wa madini ya dhahabu mkoani Geita.
Katibu Mkuu wa Chama cha Wachimbaji Madini Wanawake Tanzania (TAWOMA) Salma Ernest amebainisha hayo kwenye Semina maalumu kwa wachimbaji Wanawake katika maonesho ya nane ya Teknolojia na Uwekezaji katika sekta ya madini kwenye viwanja vya Dkt Samia Suluhu Hassan Manispaa ya Geita nakwamba hatua hiyo itawasaidia wanawake kufanya shughuli zao kitaalamu tofauti na ilivyokuwa awali ambapo baadhi walitegemea imani za kishirikina katika uchimbaji.

Baadhi ya wachimbaji wadogo Wanawake wa Mkoa wa Geita akiwemo paskazia Philbati na Asia Masimba wamesema kutolewa kwa vifaa hivyo na mafunzo mbalimbali ambayo wanaendelea kuyapata kumewafanya kuongeza ujuzi na ufanisi katika shughuli hizo.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Venas Mwase, amesema serikali imenunua mitambo 15 kwa ajili ya wachimbaji wadogo na itaendelea kuwaunga mkono.

Maonesho ya 8 ya Teknolojia na Uwekezaji katika Sekta ya Madini yanafanyika kuanzia Septemba 18–28, 2025 katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Bombambili, Manispaa ya Geita, yakitoa fursa ya kunufaika na teknolojia za kisasa kwa wachimbaji wote.