Storm FM

Miaka 25 ya GGML, kushiriki maonesho ya 8 ya madini Geita

17 September 2025, 2:09 pm

Mkuu wa mkoa wa Geita akiwa na baadhi ya wafanyakazi wa GGML katika viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan eneo la Bombambili manispaa ya Geita. Picha na mwandishi wetu

Kila mwaka mkoa wa Geita umekuwa ukifanya maonesho ya teknolojia na uwekezaji katika sekta ya madini, ikiwa ni fursa adhimu ya kukutanisha wafanyabiashara na wachimbaji wa madini kutoka maeneo mbalimbali.

Na: Ester Mabula

Geita Gold Mining Limited (GGML), kampuni tanzu ya AngloGold Ashanti, imethibitisha kushiriki kikamilifu katika Maonesho ya 8 ya Teknolojia ya Madini yanayotarajiwa kufanyika katika viwanja vya Bombambili, mkoani Geita kuanzia tarehe 18 hadi 28 Septemba 2025. Mbali na ushiriki wake, GGML pia imetoa udhamini wa Shilingi milioni 200 za Kitanzania, ikiwa ni sehemu ya mchango wake katika mafanikio ya maonesho hayo muhimu.

Kampuni hiyo, ambayo mwaka huu inaadhimisha miaka 25 tangu ianze shughuli zake nchini Tanzania, imeendelea kuwa mdau mkubwa wa maendeleo ya sekta ya madini na kusaidia maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika mkoa wa Geita ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara, kusaidia upatikanaji wa maji kwa wanachi na kuchochea ufaulu wa wasichana shuleni kwa kutoa elimu ya uzazi na taulo za kike.

Mkoa wa Geita umejipambanua kama kitovu cha uchimbaji wa madini nchini Tanzania, huku shughuli hizi zikichangia ukuaji mkubwa wa uchumi wa ndani. Kupitia kampuni kama GGML, maendeleo ya elimu, miundombinu bora, na fursa za ajira zimeendelea kuongezeka, hivyo kuimarisha maisha ya wakazi wa Geita na maeneo jirani.

Maonesho haya ya Teknolojia ya Madini ni jukwaa mahsusi linalowakutanisha wadau mbalimbali wa sekta hii – wakiwemo wachimbaji wakubwa na wadogo, watoa huduma, taasisi za serikali, wataalamu wa teknolojia, pamoja na jamii kwa ujumla – kwa lengo la kubadilishana maarifa, kuonesha ubunifu, na kujadili mbinu bora za kuongeza tija katika sekta ya madini.

GGML itatumia fursa hii kuonesha teknolojia mpya, mbinu bunifu za kuongeza ufanisi katika shughuli zake, pamoja na kuonesha vipaumbele vyake katika maeneo ya usalama, ushirikiano, na ubora wa kazi. Maonesho haya pia yataangazia mafanikio ya GGML katika miaka 25 ya uwepo wake Tanzania, hususan katika kusaidia maendeleo endelevu ya jamii inayouzunguka mgodi huo.

Akizungumza kuelekea maonesho hayo, Meneja Mwandamizi wa GGML anayeshughulikia masuala ya Uendelevu, Gilbert Mworia, alisema:

“Kushiriki katika Maonesho ya Teknolojia ya Madini kwa mwaka huu ni fursa ya kutafakari miaka 25 ya ushirikiano wetu na mchango katika sekta ya madini. Watu na taasisi nyingi zinazoshiriki katika shughuli zetu pia zitakuwepo kwenye tukio hili. Ushiriki wetu unathibitisha umuhimu wa ushirikiano na ubunifu endelevu katika kuimarisha ukuaji wa sekta ya madini.”

Kwa upande wa wananchi wa Geita, maonesho haya yanaendelea kuwa chanzo cha maarifa, fursa za kiuchumi na majukwaa ya kujifunza zaidi kuhusu sekta ya madini. Bi. Zainabu John, mkazi wa Kata ya Kalangalala, alisema:

“Kila mwaka haya maonesho yanapofanyika hapa Geita, tunajifunza mambo mengi kuhusu teknolojia za kisasa kwenye uchimbaji na namna makampuni kama GGML yanavyosaidia jamii. Pia ni fursa ya sisi wafanyabiashara wadogo kupata wateja wengi na kipato kuongezeka. Tunashukuru sana kwa uwepo wa GGML na makampuni mengine, kwani yanatuinua sisi wananchi wa kawaida.”

Maonesho haya yanatarajiwa kuvutia washiriki kutoka pande zote za mnyororo wa thamani wa madini – kuanzia wachimbaji, wasambazaji wa vifaa, watoa mafunzo, wataalamu wa mazingira, hadi watunga sera – kwa pamoja wakishirikiana kuimarisha sekta ya madini nchini Tanzania kwa njia endelevu, salama na yenye tija.