Storm FM
Storm FM
22 July 2025, 10:02 pm

Kwa mujibu wa baadhi ya raia wa Burundi wameiambia Storm FM kuwa wanakimbilia mkoa wa Geita kwa kuwa una fursa lukuki za kiuchumi.
Na Mrisho Sadick:
Wananchi mkoani Geita kwa kushirikiana na Idara ya Uhamiaji wamefanikiwa kuwakamata raia wa kigeni 54 waliokuwa wameingia nchini kinyume cha sheria, wengi wao wakitokea katika mataifa jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Burundi.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhamiaji mkoani Geita, James Mwanjotile, amewapongeza wananchi kwa ushirikiano wao mkubwa kwa Idara hiyo kwa kufanikisha oparesheni ya kuwakamata raia hao, amesema hatua hiyo imeonyesha namna ambavyo wananchi wakielimishwa huweza kuwa sehemu muhimu ya kulinda usalama na mipaka ya nchi.
Wiki iliyopita Idara ya Uhamiaji mkoani Geita ilifanikiwa kuwakamata nakuwarudisha makwao raia 126 wa Burundi walioingia nchini kinyume cha sheria ikiwa ni sehemu ya opereshani mbalimbali zinazoendelea kufanywa na idara hiyo kwa madai ya uwepo wa wimbi la raia wa kigeni ambao wanaishi kinyume cha sheria nchini.

Hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu zaidi ya raia wa kigeni 500 kutoka mataifa ya afrika mashariki wamekamatwa mkoani Geita nakurejeshwa makwao kutokana na oparesheni mbalimbali zinazoendelea kufanya idara hiyo kwa kushirikiana na wananchi wa Mkoa wa Geita.
Kwanini raia wengi wa Burundi wanakimbilia mkoani Geita?
Kwa mujibu wa baadhi ya raia wa Burundi wameiambia Storm FM kuwa wanakimbilia mkoa wa Geita kwakuwa una fursa lukuki za kiuchumi, hususani katika sekta ya uchimbaji wa madini ya dhahabu.
Maeneo mengi ya Geita yana migodi ya wazi inayotoa ajira zisizo rasmi, ambazo ni rahisi kuingia bila masharti magumu, jambo linalowashawishi raia wa kigeni kuingia kinyemela ili kutafuta kipato kwani kwa wahamiaji wanaotokea nchi zenye changamoto za ajira na uchumi hafifu kama Burundi na DRC, Geita huonekana kama eneo la matumaini mapya ya kujikwamua kimaisha.
Pia, mazingira ya kijamii na kijografia ya Geita yamekuwa kirahisi kwa wahamiaji kuvuka mipaka bila kugundulika Mkoa huu unapatikana karibu na mipaka ya nchi za Maziwa Makuu, jambo linalorahisisha usafiri usiyo rasmi kupitia njia za panya, hasa kwa wale wanaokimbia hali ngumu ya maisha au migogoro ya kisiasa katika nchi zao.
Vilevile, baadhi ya wakazi wa Geita wamekuwa wakitoa hifadhi kwa wageni hao kwa sababu ya ukarimu wa Kitanzania, jambo ambalo, ingawa ni la kibinadamu, limekuwa likitumiwa vibaya na baadhi ya wahamiaji hao wasiofuata sheria za uhamiaji.