

18 March 2025, 2:49 pm
Alama za barabarani hutajwa kusaidia katika muongozo wa matumizi ya barabara sambamba na kurahisisha watumiaji kuepukana na ajali za barabarani.
Na: Kale Chongela – Geita
Wananchi wa mtaa wa Nyantorotoro B eneo la Uboani, kata ya Nyankumbu, halmashauri ya manispaa ya Geita wamedai kukabiliwa na changamoto ya ukosefu wa alama za barabarani katika eneo hilo jambo ambalo linawapa wakati mgumu wakati wa kuvuka.
Wakizungumza na Storm Fm Marchi 17, 2025 baadhi ya wananchi wa eneo hilo wameeleza kuwa kutokuwepo kwa alama ya watembea kwa miguu inasababisha baadhi ya wananchi kuvuka eneo hilo kwa wasiwasi huku wakiomba serikali kutatua changamoto hiyo.
Mkuu wa kitengo cha matengenezo kutoka ofisi ya Meneja wa TANROADS mkoa wa Geita Mhandisi Fredrick Mande amekiri kuwepo kwa ukosefu wa alama hizo za wavuka kwa miguu na kueleza kuwa bado matengenezo yanaendelea kufanyika katika barabara hiyo kwani mkandarasi anayetekeleza uboreshaji wa lami bado hajakamilisha.