

25 February 2025, 3:06 pm
Hatimaye wananchi wa kata 8 za wilaya ya Geita na Chato wamepata neema ya kuondokana na changamoto ya muda mrefu ya ukosefu wa maji safi na salama.
Na: Edga Rwenduru – Geita
Wakazi zaidi ya laki mbili kutoka kata 8 za wilaya ya Geita na Chato mkoani Geita wameondokana na changamoto ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji safi na salama baada ya serikali kutekeleza mradi mkubwa wa bilioni 6.6 kutoka ziwa Victoria.
Hayo yamebainishwa katika ziara ya mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM Taifa Evarist Gervas wakati akizungumza na wakazi wa mamlaka ya mji wa katoro wilayani Geita ambapo amesema Dkt. Samia Suluhu Hassan amevuka lengo la utekelezaji wa miradi ya kimkakati ikiwemo wa maji kutoka Chankorongo Ziwa Victoria utakaonufaisha zaidi ya kata nane katika miji ya Katoro Geita na Buseresere Chato mkoani Geita.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Geita Barnabas Mapande amesema mradi huo wa Chankorongo ulikwama tangu miaka ya 1970 lakini kwa kipindi cha uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan mradi huo umekamilika.
Baadhi ya wakazi wa mji wa Katoro wameipongeza serikali kwa kutekeleza mradi huo wa maji huku mwakilishi wa mkuu wa wilaya ya Geita Kassim Ramadhani akisema serikali imetoa zaidi ya bilioni 1 kwa ajili ya ujenzi wa barabara za mitaa katika mji wa katoro.